Tikitimaji Zao ambalo laweza kukupa mamilioni ndani ya siku 75.



UTANGULIZI

Matikiti maji hulimwa kama zao la biashara katika sehemu nyingi duniani zenye hali ya hewa ya joto la wastani, zao hili huwapatia watu kipato. 

Matikiti maji ni mojawapo ya jamii za matunda au mbogaboga inayotambaa. Mimea hii inapatikana katika kundi linalojumuisha mimea mingine kama matango na maboga, zao la tikiti maji ni mojawapo ya zao ambalo lina faida kubwa sana ukilinganisha na mazao mengine ya muda mfupi.

Katika shamba la ukubwa wa ekari moja iliyoandaliwa vizuri na kuhudumiwa vizuri mkulima ana uwezo wa kuvuna kiasi cha Tani 15-36

HALI YA HEWA

Mimea hii husitawi maeneo yenye joto la wastani wa nyuzi kati ya 21-30 sentigredi, Iwapo mitikiti yatapandwa katika maeneo yenye joto chini ya nyuzi 15 za sentigrade huchelewa kuota.

kwa upande wa mvua matikiti yanahitaji kiasi cha mvua kati ya millimita 400-600 kwa msimu. Mvua nyingi husababisha uwepo wa magonjwa ya fangasi na bakiteria ambayo huathili mavuno.

HALI YA UDONGO

Huhitaji udongo wenye rutuba nzuri ulio na virutubisho. Vile vile hayahitaji udongo wenye kiasi kikubwa cha tindikali na alikali kubwa. Hali ya udongo kipimo cha pH iwe kati ya 6.0 na 7.0. Ingawa mmea una uwezo vile vile wa kuhimili kwenye udongo wenye PH 5.0

MAENEO YANAYOFAA KWA KILIMO CHA MATIKITI MAJI TANZANIA.

Kwa upande wa Tanzania matikiti maji hustawi vizuri kwenye ukanda wa mwinuko kidogo mikoa kama Dar es salaam, Tanga, Morogoro, Mtwara, Lindi na Pwani  ijampo zao hili hulimwa mikoa mingine pia muda mzuri wa kupanda ni kipindi cha kipupwe mwezi wa tatu mpaka wa tisa.

UANDAAJI WA SHAMBA

Kabla ya kupandikiza udongo utifuliwe vizuri na majani yaondolewe kabisa. Shamba liandaliwe vizuri kwa kusafisha ili kuondoa mimea mingine ambayo inaweza kuwa ni chanzo cha magonja.

UPANDAJI

Katika shamba la ukubwa wa hekta moja kiasi cha kilo 3-4 cha mbegu kinaweza kutumika. Panda mbegu 2 au 3 moja kwa moja katika kila shimo. Usipande katika kitalu kwasababu miche ya mitikiti huwa ni dhaifu sana wakati wa upandikizwaji iwapo itapandwa kwenye kitalu hivyo kupelekea kufa kwa miche hiyo. Panda umbali wa sentimeta 2 chini ya udongo kwa umbali wa sentimeta 30 kutoka shina hadi shina na mita 1.5 - 2 kutoka mstari hadi mstari. Zingatia kutokutumia mbegu za tikiti za kukamua kwasababu zinaweza kuwa ni chotara (Hybrid) ambayo hupelekea kushusha kiasi na ubora wa matikiti yatakayo zaliwa kwa sababu yatakuwa ni kizazi cha pili (F2)

MATANDAZO (MULCHES 

Matandazo unaweza kutumia nyasi na mabaki ya mimea mingine kufunika aridhi. Baada ya miche kutambaaa kwa kiasi unaweza kuweka matandazo (mulches) ambayo yaweza kuwa nyasi kavu kwenye udongo ili kuzuia upotevu wa unyevu vile viile kupunguza uotaji wa magugu shambani kwako. Vile vile matandazo yakioza yanaongeza rutuba kwenye udongo na hulinda udongo dhidi ya mmomonyoko wa udongo.

UWEKAJI WA MBOLEA

Mbolea za viwandani aina ya NPK au mbolea zenye nitrogen kiasi cha gramu 10 hadi 20 ziwekwe wakati mimea ikiwa ni midogo mpaka pale maua ya kike yatakapoanza kuonekana. Vilevile samadi inaweza kuwekwa wakati mimea ikiwa midogo. Baada ya mimea kutengeneza matunda weka mbolea aina ya urea na potassium hadi mara 2 au 3 kwa wiki mpaka matunda yatakapokomaa.

UMWAGILIAJI

Shamba linatakiwa limwagiliwe mara kwa mara wakati mvua zinapokosekana au wakati wa mvua chache. Kipindi muhimu zaidi ambapo mimea hii huhitaji maji ni katika kipindi cha uotaji wa mbegu, wakati wa kutoa maua na siku takribani kumi kabla ya kuvuna. Iwapo kutakuwa na ukosefu wa maji kutasababisha kutengenezwa kwa matunda ambayo si mazuri na yenye umbo baya wakati wa utengenezaji wa matunda pia upunguaji wa ukubwa wa tunda.

Angalizo; usimwagilie matikiti wakati wa jioni sana au usiku kwasababu inaweza kusababisha magonjwa ya majani kutokana na unyevu kukaa muda mrefu. Vile vile usimwagilie juu ya maua wakati wa asubuhi au join kwasababu unaweza kuzuia wadudu kama nyuki ambao ni muhimu sana wakati wa uchavushaji.

MAUA NA MATUNDA

Matikiti hutoa maua dume na jike kwenye tawi moja. Kwa kawaida maua dume huwa ni madogo zadi na hutoka mapema zaidi yakifuatiwa na maua jike ambayo huwa makubwa zaidi. Maua yanaweza yasionekane au yasitokee iwapo kiasi kidogo cha maji kitamwagiliwa ,upungufu wa viritubisho kwenye udongo na hali ya hewa ya joto/baridi sana n.k

Uchavushaji hufanya na wadudu na iwapo itaonekana hakuna wadudu unaweza kuchavusha kwa kutumia mkono.

Hii hufanywa kwa , kukata maua dume kwa kisu na kufanya uchavushaji kwenye maua jike, maua jike ya mwanzo kwenye tawi ndiyo yenye ukuaji bora zaidi, unaweza kukata tawi lisiendelee kukua baada ya matunda kutokeza hii husababisha kuwa na matunda makubwa zaidi. Hii inawezwa kufanywa zaidi wakati wa Asubuhi.

MAGONJWA NA WADUDU

Wadudu wa matikiti wako wa aina mbalimbali kuna wanaoshambulia majani na maua, na wengine hushambulia matunda , pia kuna magonjwa ya fangasi ambayo hushambulia mimea. Magonjwa kama Ukungu wa unga (powdery mildew) na wa chini (Downy mildew) na mengine yathibitiwe kabla hayajaleta madhara kwenye mimea. Ili kujua dawa za magonjwa ni vizuri kuchukua sampuli na kwenda nayo kwenye duka la dawa na pembejeo za kilimo ili kupata dawa sahihi. Dawa aina ya mancozeb inaweza kutumiwa kuthibiti ugonjwa magonjwa hayo hapo juu.

Vilevile matikiti hushambuliwa na wadudu ambao hukaa katika majani, maua na matunda.

Sumu aina ya Karate itasaidia kuua wadudu wa majani, maua na matunda.

UVUNAJI MATIKITI

Kabla ya kuvuna matunda ni vema kwanza kujua kuwa matikiti huchukua takribani miezi mitatu mpaka mitano toka inapopandwa mpaka kukomaa. Hii hutegemea na aina ya matikiti yenyewe. Tikiti lililo komaa linaatakiwa na mwonekano wake huwa kama ifuatavyo;

✅ Rangi ya mng’ao hupotea

✅ Upande wa chini wa tunda huanza kuwa na rangi ya njano

✅ Kikonyo juu ya tunda hukauka kabisa na kuwa kijivu.

✅ Njia nzuri ni kuyapiga kwa kiganja na kusikiliza mlio wake unakuwa kama mlio wa ngoma.

N:B Tumia kisu wakati wa kuvuna matikiti, yabebwe na kuhifadhiwa vizuri kwenye makasha tayari kuuzwa au kwa matumizi binafsi.

MASOKO

Ukubwa wa tikiti na mwonekano wake ni baadhi ya sifa zinazoangaliwa na wananuzi. Matikiti madogo sana huwa hayapendi sana na wanunuzi. Kwa Tanzania wakulima wengi wanauza matikiti katika masoko ya ndani yanayopatikana takribani nchi nzima. Kwa miaka kadhaa tikiti moja limekuwa likiuzwa kwa wasitani wa Tsh. 1000/= kwa tikiti dogo mpaka Tsh. 3000/= kwa tikiti kubwa katika masoko.

MAVUNO

Mavuno ya matikiti yanategeme huduma za shamba pamoja na hali ya hewa, matikiti pia hutofautiana katika mavuno kulingana na aina ya matikiti. Kwa wastani matikiti yanaweza kutoa mavuno kati ya Tani 15-36 kwa ekari moja.

Youtube channel  Subscribe here