Kilimo cha Migomba/ Ndizi

NADHARIA YA KILIMO CHA MIGOMBA/NDIZI KWA UFUPI

Migomba hukua vizuri sehemu zenye joto kidogo na unyevu nyevu na mwinuko wa 0 -1800 mita kutoka usawa wa bahari. Aina nyingine za migomba huweza kusitawi hadi kwenye mwinuko wa mita 2100 kutoka usawa wa bahari.

Mahitaji ya mvua ni ya wastani wa mililita 1000 kwa mwaka japokuwa migomba husitawi vizuri kama ikipata maji ya kutosha. Hii ni pamoja na kumwagilia kipindi cha kiangazi bila kutuamisha maji.  Halijoto ya 27°C hadi 38°C ndio ifaayo kwa kilimo cha ndizi na migomba hudumaa kama kuna baridi sana (chini ya 13°C.)

Upepo mwingi ni tatizo kwa migomba kwa kuchana majani na kuyaharibu pia kuangusha migomba. Kupanda migomba kwa vikundi husaidia kuzuia upepo na ikibidi migomba iliyobeba ndizi iwekewe nguzo kama zinapatikana.

Udongo mzuri kwa kilimo cha ndizi ni tifutifu yenye uwezo wa kupitisha maji na hewa kwa urahisi. Udongo wenye mbolea nyingi ni mzuri sana kwa migomba.

Migomba (Ndizi) hupandwa kwa kutumia vichipukizi ama migomba midogo ama sehemu za viazi zenye uwezo wa kutoa vichipukizi. Uzao wa ndizi hutegemea sana aina na umri wa vichipukizi vilivyotumika wakati wa upandaji. Vichipukizi vizuri ni vile vilivyochongoka vyenye urefu wa sentimeta 75 na upana wa chini ya shina wa sentimeta 15 na majani yake yamechongoka. Hivi huzaa baada ya miezi 18 tangu kiypandikizwa. Vipandikizi hutoa ndizi hata baada ya miaka 2-3. Migomba mikubwa wastani huzaa bada ya miezi 5-8. Vichipukizi maji vyenye majani mapana havifai kwa kupandikiza kwani huzaa ndizi ndogo na uwezekano wa kupona baada ya kupandikizwa ni mdogo.

Upandaji wa migomba.

Miche ama vichipukizi vya migomba vipandwe kwenye shimo lenye urefu wa sentimita 60 na upana wa sentimita 60. Udongo uchanganywe vizuri na mbolea ya kutosha. Kama mvua hazitoshi, shimo liwe na urefu wa sentimita 150 na upana wa sentimita 100.

Nafasi za kupanda

Kwa aina za migomba midogo nafasi kutoka mmea hadi mmea iwe mita 3, na kutoka mstari hadi mstari iwe mita 3. Migomba 1000 kwa ekari. Kwa aina ndefu. Mmea hadi mmea mita 3 na mstari hadi mstari mita 4. Migomba 480 kwa ekari.

Muda wa kupanda Migomba

Muda muafaka ni mwisho wa msimu wa kiangazi ama mwanzo wa msimu wa mvua.

Youtube channel  Subscribe here